Africa Inland Church Tanzania, ilianzishwa katika kijiji cha Nassa, Mwanza mwaka 1909. Mapema mwaka 1887 wamisionari kutoka Church Missionary Society (CMS) walifika katika Kijiji cha Nassa kufungua kanisa. Kwa zaidi ya miaka ishirini wamisionari wa CMA walikuwa wamehudumu katika ukanda wa Ziwa Viktoria (Wakati huo ikiitwa Tanganyika) wakifungua makanisa. Lakini kutokana na sababu mbalimbali, waliamua kuhamia Uganda. Wamisionari hao hawakutaka kuacha kutaniko hilo changa, hivyo walitafuta mtu wa kuendeleza kazi kutoka pale walipofikia.
Africa Inland Mission (AIM) iliyokuwa tayari ikifanya kazi nchini Kenya iliombwa na CMS kutuma mmishonari nchini Tanganyika. Tarehe 29 Juni 1909 Mchungaji (Rev). Emil Sywulka na mke wake Bi. Marie Sywulka walipokelewa na wamisionari wa CMS huko Nassa kuendeleza huduma za kiroho.Kazi iliendelea chini ya mch Emil Sywulk na Makanisa mengi yalifunguliwa na Mission ikaendelea, Mfano Mwanza walianzisha mwaka 1912.
Mwaka 1937-1956 kanisa lilibadilishwa jina na kupewa jina la EKLEZIA EVANJELI YA KRISTO (E.E.K) likiwa na katiba iliyowapa mamlaka na kanuni tatu; 1.Kujitawala lenyewe 2.Kujitegemea lenyewe 3.Kujieneza lenyewe. Jina la kanisa EKLEZIA EVANJELU YA KRISTO (EEK) lilibadilishwa jina tena mwaka 1957 na kuitwa AFRICA INLAND CHURCH TANGANYIKA.
Kanisa la AIC Tanganyika lilianza kujiongoza tarehe 12/2/1960 katika mkutano wa Synod na Field Council wakati huo mkuu wa kanisa akiitwa DIRECTOR yaani Mkurugenzi. Mkurugenzi wa kwanza AICT ni Mchungaji Jeremia Mahalu Kisula ambaye pia baadaye alikuwa Askofu wa kwanza wa kanisa. Askofu wa sasa ni Mussa Masanja Magwesela (pichani)
HISTORIA FUPI YA KANISA LA AIC-TANZANIA
MALENGO YA AIC TANZANIA
- Kumpenda, kumwabudu na kumtukuza Mungu.
- Kueneza injili ya Bwana Yesu Kristo popote Tanzania, Afrika na duniani kote.
- Kufundisha watu Neno la Mungu na kuwabatiza wale wanaomwamini Bwana Yesu Kristo.
- Kufungisha ndoa za Wakristo ambao ni wafuasi wa AICT na wenzi wao ambao ni wafuasi wa makanisa mengine yenye imani sawa na AICT, ambao hawana lawama katika kanisa na kuwabariki watoto wao.
- Kuendesha ibada ya mazishi kwa misingi ya Biblia na taratibu za huduma za AICT.
- Kuwashirikisha Wakristo wote katika kazi za Kanisa na Taifa, Kiroho na Kimwili na kiakili.
- Kufanya mikutano ya uamsho wa kiroho hasa kuhubiri Injili
- Kumwomba Mungu mahitaji mbalimbali.
- Kuhudumia watu kiroho, kimwili na kiakili katika mazingira yao:
- Huduma za kiroho;
- Huduma za kimwili, kiakili na kimazingira;
ASKOFU WA SASA
Mussa Masanja Magwesela
HISTORIA FUPI YA KANISA LA AICT KIBADA
Kuanzishwa, maendeleo ya Kanisa na Uongozi
Kanisa la AICT Kibada lilianza mwezi Novemba 2012, katika kitongoji cha Mwera baada ya msiba wa muumini mmoja Bw. Modekai, aliyetafuta huduma za kiroho kwa mazishi ya mwanaye. Pastoreti ya Kigamboni ikiongozwa na Mchungaji Emmanuel Mchembe, ilimtuma Mwinjilisti Emmanuel Jeremia Itogelo ambaye baadaye aliendela kutoa huduma mahala hapo kukiwa na waumini wa kaya 4.
Katika Ibada ya Krismasi ya 25/12/2012, iliyofanyika katika kanisa la AICT Mbutu. Mchungaji Emmanuel Mchembe alitangaza rasmi kuanza kwa Kanisa la la AICT Kigamboni katika kitongoji cha Mwera, chini ya huduma ya Bw. Joshua Jimoku akiwa mwenyekiti wa Vijana na Mwenyekiti wa Injili wa Pastoreti ya Kigamboni.
Kanisa hilo baadaye lilihamia katika kitongoji cha Milungu baada ya Mama Debora kujitolea kiwanja chake. Kanisa la AICT Kibada liliongozwa na Mwinjilisti (kwa sasa Mchungaji) Emmanuel Jeremiah Itogelo aliyehudumu kuanzia tarehe13 Oktoba 2013 hadi tarehe 27 Machi 2016. Wakati huo wazee wa kanisa walikuwa:
(i) Bi. Dotto Butakilaga Kasule na
(ii) Bw. Rogers Msobi.
Mnamo mwaka 2016 alitumwa Mwinjilisti Aloys Singu kuhudumu katika kanisa la AICT Kibada akitokea Pastoreti ya Chang’ombe. Mwinjilisti Singu alihudumu kuanzia April 2016 hadi Agusti 2018. Mwinjilisti aliongoza kanisa ambalo baada ya ujenzi kukamilika, lilihamia kutoka kitongoji cha Milungu hadi lilipo sasa Mtaa wa Sokoni, kitongoji cha Kigora- Kibada waliponunua kiwanja cha Kanisa kwa juhudi za watumishi waliokuwepo na viongozi wengine waliokuwa wakisimamia Kanisa wakati huo.
Tarehe 11 Mei 2019, Mwinjilisti Enock Makeja alianza huduma katika Kanisa la AICT Kibada. – akisaidiwa na wazee wa kanisa;
(i) Bw. Shadrack Mijinga na
(ii) Injinia Phares Ngeleja.
KANISA LA MWANZO
WATUMISHI WALIOWAHI KUHUDUMU KATIKA KANISA LA AICT KIBADA
Mwinjilisti Enock Makeja
Alihudumu Kanisa la AICT Kibada tangu Mei 2019 hadi Juni 2022.
Bi Dotto Butakilaga Kasule
Alihudumu AICT Kibada akiwa Mzee wa Kwanza wa Kanisa mwaka 2013
Mwinjilisti Joshua Jimoku
Alihudumu AICT Kibada Januari hadi Oktoba 2013
Mwinjilisti Aloys Singu
Alihudumu katika Kanisa la AICT Kibada akitokea Pastoreti ya Changombe tangu April 2016 hadi Agosti 2018.
Mwinjilisti Happiness Mungole
Alihudumu Kanisa la AICT KIbada wakati linaanzishwa mwaka 2012 hadi 2014.